Ugonjwa wa P.I.D dalili, Kinga na tiba.

Kwa Kiswahili hufahamika zaidi kama maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa uzazi wa mwanamke ikihusisha mlango wa kizazi, mji wa uzazi, mirija ya uzazi pamoja na vifuko vya mayai ya uzazi.


PID hutokea baada ya kupanda juu kwa bakteria wabaya kutoka kwenye uke na mlango wa kizazi kwenda kwenye kuta za mji wa uzazi na mirija ya uzazi.



Uambukizwaji

Neisseria gonorrhoeae, Chlamydia trachomatis na Mycoplasma genitalium ndiyo vijidudu hatari zaidi kwa kusababisha PID, na husambazwa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia ya ngono, hivyo uwepo wa magonjwa ya zinaa hasa Kisonono na Klamidia huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ugonjwa wa PID.


Mtu anaweza pia kupata ugonjwa huu kutokana na uwepo wa maambukizi makali baada ya kutoa ujauzito, kuharibika kwa ujauzito au baada ya kufanyika kwa utaratibu wowote ule unaofungua tumbo. 


Katika hali chache, bakteria wazuri wanaopatikana kwenye uke wanaweza kugeuka wabaya ikiwa watavuka mlango kwa kizazi na kuingia sehemu ya juu ya viungo vingine.


PID inaweza kusababisha ugumba, utasa, maumivu ya kudumu ya tumbo la chini na nyonga pamoja na kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi.


Ni vizuri ikishughulikiwa vizuri, mapema na kwa usahihi. 




Dalili

Dalili za ugonjwa huu hutofautiana kulingana na hatua husika. Sio kila mwanamke huonesha dalili za kufanana na mwingine.


Pamoja na uwepo wa tofauti hizi, dalili za ujumla za ugonjwa huu ni;


Maumivu makali sehemu ya chini ya tumbo

Homa kali

Kutokwa na damu katikati ya mzunguko wa hedhi

Mlango wa kizazi huwa mwekundu sana, ambao mara nyingi hutoa uchafu mzito wenye rangi ya njano-kijani

Kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi

Baadhi ya wanawake huwa hawaoneshi dalili kubwa, na hudhani kuwa wapo sawa kabisa. Changamoto huja wakati wa kutafuta ujauzito, wengi hushitushwa na ugumu katika kufanikisha zoezi hili.

Maumivu wakati wa haja ndogo na wakati wa tendo la ndoa

Tiba

PID inaweza kutibiwa kwa kutumia madawa (viua vijasumu-antibiotics) mfano Azithromycin, Ceftriaxone, Clindamycin, Gentamicin na Doxycyline.


Mhudumu wa afya atakuelekeza matumizi sahihi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.


Kinga

Njia za kujikinga na ugonjwa huu zipo wazi. Unaweza kujikinga kwa kufanya mambo yafuatayo;


Kuwa mwaminifu, tulia na mpenzi mmoja.

Wakati wa matibabu, ni vizuri ukijizuia wewe na mwenzi wako kushiriki tendo la ndoa ili kuepuka nafasi ya kuambukizana tena. Inafaa msubiri hadi ugonjwa upone.

Ili kukata mnyororo wa maambukizi, ni vizuri wapenzi wote wakitibiwa kwa pamoja. Ni muhimu kukumbuka kuwa,wanaume hawawezi kuugua PID lakini huwa na uwezo wa kubeba bakteria wanaosababisha tatizo hili na kuwapitisha kwa mwanamke wakati wa tendo la ndoa.

Muhtasari

Ni muhimu pia mwanamme akienda hospitalini kuchunguzwa pamoja na mwanamke kwani anaweza kuwa chanzo cha ugonjwa huu. (6)


Aidha, siyo kila uchafu mweupe, manjano au kijani unaotoka ukeni humaanisha PID, pia siyo kila maumivu yanayotokea chini ya tumbo, kutokwa na damu au hata uwepo wa maumivu makali wakati wa tendo la ndoa huwa wa PID.


Epuka kununua vitu dukani, mitandaoni au mtaani bila kupima kwanza hospitalini, utaumia.



Mvurugiko wa homoni (Hormonal imbalance)

Homoni au kwa lugha nyingine zikifahamika kama vichocheo vya mwili, ndiyo kemikali zinazosambaza taarifa za mwili kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.


Taarifa hizi huviamuru viungo mbalimbali vya mwili nini cha kufanya na kwa wakati gani. 


Tunaposema kuwa unasumbuliwa na tatizo la mvurugiko wa homoni (hormonal imbalance) huwa tunamaanisha kuwa, homoni fulani mwilini mwako zipo nyingi sana, au chache sana kulinganisha na kiwango sahihi kinachopaswa kuwepo. 


Mabadiliko madogo ya kiwango cha homoni kinachopaswa kuwepo mwilini kinaweza kusababisha matatizo makubwa kwenye afya ya mhusika, pamoja na utaratibu wa kawaida wa maisha yake ya kila siku. (2, 3)


Chanzo

Kuna mambo mengi yanayoweza kusimama kama chanzo cha kuvurugika kwa homoni.

Kwa kuwa mwili wa binadamu huwa na homoni nyingi zinazozalishwa na tezi tofauti tofauti, sababu au vyanzo vya tatizo hili hutofautiana pia.


Miongoni mwake ni;


Matumizi ya baadhi ya madawa, mfano bangi

Matibabu ya saratani

Uvimbe kwenye tezi za pituitary

Mkazo (stress)

Ajali

Magonjwa hasa ya kisukari na yale yanayohusisha tezi za thyroid

Umri wa ukomo wa hedhi

Ujauzito na unyonyeshaji

Matumizi ya njia za uzazi wa mpango mfano kitanzi, majira, vijiti au sindano za depo provera.

Uzito uliozidi pamoja na mtindo mbaya wa maisha hasa upande wa mlo na vinywaji

Dalili

Dalili za uwepo wa tatizo hili hutofautiana kulingana na aina ya homoni inayosumbua, sehemu ambayo homoni husika hufanya kazi pamoja na jinsia ya mhusika.


Kwa ujumla wake, tatizo hili huwa na dalili zifuatazo


Mvurugio wa mzunguko wa hedhi unaoweza kusababisha hedhi ije kubwa sana, hedhi isionekane kwa miezi kadhaa, hedhi ipotee kabisa au pia ije bila kufuata utaratibu maalum huku ikiambatana na maumivu makali sana.

Kusumbuliwa na matatizo ya usingizi 

Chunusi nyingi

Uchovu bila sababu

Kupoteza kumbukumbu haraka

Kichefuchefu, kuharisha pamoja na maumivu ya tumbo yanayotokea bila mpangilio maalumu

Kupoteza hamu ya kula

Ongezeka la ghafla la uzito wa mwili bila sababu maalum

Uke kuwa mkavu pamoja na kupungua au hata kuisha kabisa kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa

Kutokwa sana na jasho kila mara

Msongo wa mawazo

Ugumba

Kuota kwa ndevu pamoja na nywele kwenye sehemu mbalimbali za mwili (Wanawake)

Maumivu makali wakati wa tendo la ndoa

Kwa wanaume, huwa na dalili ya ziada ya kupunguza hamu na ufanisi kwenye kushiriki tendo la ndoa

Tiba

Mhudumu wako wa afya atauliza maswali kadhaa hivyo ushirikiano wa kutosha unapaswa kutolewa.


Ikiwa ataona inafaa, vipimo vitachukuliwa ili kubaini homoni zinazosumbua kwa wakati huo.


Utaratibu wa aina ya matibabu, dawa pamoja na dozi utategemea na homoni zenyewe, ukubwa wa tatizo na athari zilizopo kwa wakati huo.


Ikiwa homoni zako zitakuwa ni chache, matibabu makuu ni kupewa dawa zenye kuweka sawa homoni hizo, utaratibu ambao kitaalam huitwa Hormone Replacement Therapy ambayo inaweza kufanyika kwa njia ya sindano au vidonge.


Kwa watu wenye homoni nyingi kuliko kiwango cha kawaida, baadhi ya dawa zinaweza kutumika, upasuaji, tiba ya mionzi au mjumuiko wa njia zote unaweza kufanyika.


Baadhi ya dawa zinazoweza kutumika ni Metformin, Levothyroxine na Clomiphene citrate.


Kinga

Mvurugiko wa homoni unaweza kuwa na madhara hasi kwa afya ikiwa hautatibiwa haraka.


Kwa kuwa tatizo hili limekuwa kubwa sana siku hizi kutokana na athari za aina ya maisha tunayoishi, ni muhimu kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kubaini kama lipo, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.


Baadhi ya mambo yanayoweza kufanyika ili kujikinga na tatizo hili ni;


Kutunza uziti sahihi wa mwili

Kula mlo bora

Kufanya mazoezi ya mwili

Kudhibiti stress pamoja na kupata muda mwingi wa kupumzika

Kufuatilia tiba sahihi ikiwa unaugua magonjwa sugu

Acha kuvuta sigaara

Tatizo hili hukaribisha magonjwa sugu, pamoja na kudumaza ubora wa afya ya uzazi kwa ujumla wake.


Muhtasari

Kama unapatwa na dalili usizozielewa ni muhimu kufika hospitalini ili upats uchunguzi na tiba. Kwa kuwa homoni za mwili ni balozi mwema anayetoa taarifa mbalimbali zenye kuupa amri mwili wako, ni lazima uhakikishe zipo sawa kila muda.


Previous Post Next Post

Contact Form